VITUKO VYA MA SUPERSTAR WA BONGO

Na Imelda Mtema
STAA katika kiwanda cha filamu Bongo, Aunt Ezekiel ‘Gwantwa’ amesema kuwa, anaamini Mfalme wa Rhymes 2003, Suleiman Msindi ‘Afande Sele’ anamzimia kinoma ndiyo maana kila anapofanya mahojiano haachi kulitaja jina lake.

Nyota huyo kutoka Bongo Movie, amesema hayo kufuatia Afande kuhojiwa na gazeti ndungu na hili kuhusiana bifu lake na raisi wa Manzense kutoka Tip Top Connection, Hamad Ally ‘Madee’ ambaye alimfananisha rais huyo na Aunt Ezekiel.

“Hii siyo mara ya kwanza kwa Afande kunitaja, kila anapofanya mahojiano lazima alitaje jina langu mi ninahisi ananipenda na ni mmoja kati ya mashabiki wangu,”alisema Aunt.

Aunt ameongeza kuwa, Afande atakuwa ni mnunuaji mzuri wa filamu zake na anampenda jinsi anavyooigiza ndiyo maana akamuona anavyojipodoa hadi kumlinganisha na Madee.

“Naamini kabisa afande Sele ni mpenzi wa kazi zangu na ndiyo maana anapenda kunitaja kila anapofanya mahojiano mablimbali, najua ananikubali,”alisema Aunt

Ruth Mateleka na Gladness Mallya
KICHWA cha ukweli kinachosumbua katika Muziki wa Bongo Fleva, Mwasiti Almas (pichani) ameibuka na kutoa yake ya moyoni kuwa anahitaji mume wa kumuoa.

Katika mahojiano na kona hii juzikati, jijini Dar es Salaam, Mwasiti ambaye anasumbua vilivyo na kibao cha Siyo Kisa Pombe, alisema anamhitaji mwanaume huyo baada ya mwaka mmoja.

Imelda Mtema na Musa Mateja
Lile bifu la ‘mayanki’ wawili wa muziki wa Kizazi Kipya, Naseeb Abdul ‘Diamond’ na Rahim  Rummy Nanji ‘Bob Junior’, linazidi kuumuka ambapo wameponea chupuchupu kutwangana.

Tukio la wawili hao kutaka kutoana manundu lilijiri ndani ya Ukumbi wa New Maisha Masaki, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii.

Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na mapaparazi wetu, Bob Junior, Top C wa Sharobaro kwa kolabo na msanii wa Kundi la Dar Stamina, Nurdin Bilal ‘Sheta’, walikuwa wakiangusha bonge la shoo ‘kiwanjani’ hapo.

Katika hali ya kushangaza, ghafla ukumbini humo hali ilichafuka ambapo walizama ‘masela’ ambao kazi yao ilikuwa ni kumzomea Bob Junior katika kila kitu alichofanya.

Nyuma ya zomea zomea hiyo kuliibuka madai mazito kuwa, watu hao ambao walifika kiwanjani hapo wakiwa wamejaa kwenye gari aina Toyota Coaster walikodiwa na Diamond huko Kariakoo ili kuja kumpotezea Bob Junior.

Baadaye Bob Junior alishuka stejini na kukatiza jirani na Diamond aliyekuwa ameegemea kwenye ukuta ukumbini humo  ambapo kwa mujibu wa watu waliokuwa jirani walisikika wakibadilishana lugha ya matusi ya nguoni na vitisho vya kufa mtu.

Achilia mbali matusi waliyokuwa wakiporomosheana mithili ya mvua zinazonyesha nchini kote, Diamond aliamua kumfuata Bob Junior ‘toileti’ ili wakatwangane kumaliza ubishi unaoendelea kati yao.

Kama siyo kaka wa Bob Junior ambaye jina lake halikupatikana, leo kungekuwa na stori nyingine mbaya zaidi kama siyo maombolezo ya vifo kwani alifanya kazi ya ziada kuwazuia kutoana macho.

Habari zinadai kwamba Bifu la Diamond na Bob Junior linazidi kuumuka kila kukicha kwa kujumuisha watu wengine zaidi.

Ukiachia mbali Wema Abraham Sepetu aliyewekwa chini ya ulinzi na ‘wajeda’ wa Oysterbay wiki iliyopita kwa ishu hiyo, naye msanii Sheta anatajwa kwenye bifu hilo kufuatia kuwa kwenye ‘kampani’ ya Wasafi ambayo Diamond ndiye rais wao ikielezwa kuwa ni hasimu wa ile ya Sharobaro iliyo chini ya Bob Junior.

Bifu la Diamond na Bob Junior (wakati huo akiwa prodyuza) lilianza miezi kadhaa iliyopita baada ya rais huyo wa Wasafi kumtuhumu mwenzake kuwa alikataa kumrekodia kibao chake kipya cha Gongo la Mboto akisingizia kuumwa sikio.

NaGladness Mallya na Haruni Sanchawa
Kwa mara nyingine Miss Tanzania ‘The history’ 2006/07 ambaye kwa sasa ni moto wa kuotea mbali katika Bongo Movies, Wema Abraham Sepetu, ameshikiliwa na polisi katika Kituo cha Oysterbay Kinondoni, Dar es Salaam kwa saa kadhaa kwa ajili ya mahojiano. Uchunguzi wa Risasi Jumamosi umefanikisha kupatikana kwa chanzo cha mrembo huyo kushikiliwa na ‘wajeda’ kuwa ni kutoa lugha chafu na vitisho kwa Prodyuza wa Studio na Lebo ya Sharobaro, Rahim  Rummy Nanji ‘Bob Junior’.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar juzi, Bob Junior alidai kuwa Aprili 11, mwaka huu saa 12 jioni, Wema alimpigia simu na kumporomoshea mvua ya matusi makubwa ikijaziwa na vitisho vya kufa mtu. Rais huyo wa Masharobaro aliendelea kushusha tuhuma kuwa, mbali na kumtishia aliahidi kumtafutia mabaunsa ili ‘wamruke ukuta’ jambo ambalo hakuwa tayari kukutana nalo hivyo aliona njia pekee ya kukwepa ‘sheshe’ hilo ni kukimbilia polisi.
Bob Junior alisema alimfungulia Wema jalada la kesi namba OB/RB/6337/2011-KUTISHIA MAISHA.

WEMA CHINI YA ULINZI
Ilielezwa kwamba, baada ya Bob Junior kufungua kesi hiyo, Wema naye alifika kituoni hapo kwa nia ya kufungua kesi kwa ajili ya rais huyo wa masharobaro ambapo aliambiwa na polisi kuwa yuko chini ya ulinzi kwa mahojiano.

Wema alidaiwa kukaa kituoni kwa zaidi ya saa 3, Aprili 13, mwaka huu hadi alipofika mwimbaji wa FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’, Patcho Mwamba na kumwekea dhamana.

Wema  aliachiwa huru kwa masharti ya kuripoti kituoni hapo Aprili 14, mwaka huu saa 2:30 asubuhi.

Risasi Jumamosi lilifika kituoni hapo na kumshuhudia Wema akitinga eneo hilo saa 3:30 asubuhi akifuatana na wasanii wenzake wa filamu, Rose Donatus Ndauka na Jacqueline Steven Pentezel ‘Jack wa Chuz’.

Hata hivyo, mapaparazi wetu walipojaribu kuzungumza nao, Jack wa Chuz alijibu kwa niaba ya Wema aliyegoma kuzungumza na kusema kuwa walifika eneo hilo kuchukua kibali cha ‘kushuti’ filamu.

Habari za ndani zilidai kuwa, Wema na Bob Junior walikalishwa chini kituoni hapo na kutakiwa kumaliza tofauti zao lakini prodyuza huyo alikataa na kutaka ishu iende mahakamani.
KWA NINI WEMA NA BOB JUNIOR?

Chanzo cha yote hayo ni bifu linaloendelea kati ya Bob Junior na msanii Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambaye ni laaziz wa Wema ikielezwa kuwa prodyuza huyo alimdhalilisha mrembo huyo hivyo naye akataka kulipiza.

Mara ya kwanza Wema alikaa nyuma ya nondo za mahabusu mwaka 2009 akikabiliwa na shitaka la kuvunja kioo cha gari la staa wa filamu, Steven Charles Kanumba.

Na Rhobi Chacha
Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu bila kuanika sababu ya kumwagana na aliyekuwa mpenzi wake, Rehema Chalamila ‘Ray C’, hatimaye mwanahip hop wa Kundi la Nako 2 Nako, Isaack Waziri Makuto ‘Lord Eyez’ameibuka na ‘kufyatuka’ kilichosababisha wakatemana. Akizungumza katika mahojiano maalum na Paparazi wetu kwa njia ya simu juzi, Lord Eyez alisema kuwa, kwa sasa ana majukumu lukuki kutokana na akili yake yote kuegemea kwenye kazi na kuachana na starehe kama ilivyokuwa enzi hizo akiwa na Ray C.

Jamaa alimfyatua Ray C kwa kudai kuwa, wakati akiwa kwenye ‘malavidavi’ na mrembo huyo au Kiuno Bila Mfupa, alikuwa hafanyi kitu chochote cha kimaendeleo hivyo kusababisha kushuka kiutendaji.

Lord Eyez aliendelea kuweka wazi kuwa, kuendekeza starehe ilikuwa ni moja ya sababu za kumwagana na Ray C na nyingine ni kero za hapa na pale za kimapenzi zilizokuwa zikijitokeza kila kukicha.

Siwezi kurudia kosa, cha msingi ni kuangalia majukumu ya kazi yangu, sihitaji tena starehe za wanawake kwani vitu kama hivyo ukiviendekeza ‘utalosti’ na ukizingatia hivi sasa kundi letu la Nako 2 Nako tunatayarisha video ambayo ifikapo Juni itakuwa kitaani,” alisema Lord Eyez ikiwa ni mara ya kwanza kutoa tamko kama hilo.

Alimalizia: “Mapenzi na Ray C yalinifanya nikajisahau kwenye fani ila niliamua kutengana naye ili kila mmoja awe kivyake, kilichobaki ni urafiki wa kawaida na sidhani kama tunaweza kurudiana.”

Jitihada za kumpata Ray C hazikuzaa matunda baada ya kilongalonga chake cha kiganjani kutokuwa hewani kila alipotafutwa.

Lord Eyez na Ray C walikuwa wapenzi ambao walifikia hatua ya kuoana ila walimwagana ghafla mwaka jana huku mwanahip hop huyo akigoma kutoa sababu ya kuachana kwao.

Na Shakoor Jongo
PICHA zenye pozi lenye utata za mastaa wa kiwanda cha filamu za Kibongo, Steven Charles Kanumba na Aunt Ezekiel Grayson juzi kati zilinaswa na kushikiliwa mikononi mwa gazeti hili kwa kile kinachodaiwa kuwa, ilikuwa zisambazwe kwenye mitandao mbalimbali duniani.

Kikizungumza na Ijumaa Wikienda, chanzo chetu cha habari kilisema kuwa, picha hizo zilinaswa kutoka kwa mtu mmoja ambaye alikuwa akizipiga bei.

“Unajua mimi namiliki mtandao ambao unajihusisha na habari za mastaa, sasa baada ya kuletewa ili nizinunue kwa kweli nilishtuka sana kwani sikutegemea mtu kama Kanumba angeweza kupiga picha hizi, lakini  kwa Aunt sikushangaa,” kilisema chanzo hicho.

Kumekuwa na habari zenye utata kuwa, picha hizo zilipigwa na Mtasha mmoja aliyedai ni kwa lengo la kutoa kwenye tangazo moja la kibiashara.

Hata hivyo, habari nyingine zinadai kuwa, wawili hao walipiga picha hizo kwa lengo la kulipwa ujira.

Madai hayo yanasindikizwa na kauli ya chanzo chetu ambapo kinasema: “Si wawili hao tu waliopiga picha za staili hiyo kwani nina orodha ya mastaa wengine wa Bongo ambao nasikia hulipwa ujira mdogo kwa kukubali kupigwa picha kama hizi.”

Kikaendelea: “Unajua staa wa Ulaya hadi akubali kupiga picha kama hizi basi ujue amevuta mkwanja mrefu sana lakini kwa hawa wetu hulipwa vijisenti tu vya kubadilishia mboga au kununulia nguo.”

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusiana na picha hizo.
Ijumaa Wikienda linaendelea kuchimba zaidi ili kujua kilicho nyuma ya picha hizo na kuwaletea wasomaji wetu.

Na Gladness Mallya
Urafiki uliochipukia hivi karibuni kati ya mastaa maarufu wa filamu Bongo, Wema Sepetu, Rose Ndauka na Jacqueline Pentezel, umezua mjadala huku wadau wakidai eti una harufu ya damu, Ijumaa Wikienda linakumegea.

Wakizungumza na paparazi wetu katika nyakati tofauti, baadhi ya mastaa wanaowafahamu vizuri wasanii hao walioanzisha kampuni yao iitwayo JAROWE walidai kuwa, kutokana na tabia zao kuna uwezekano siku moja wakatibuana.

“Mimi nawafahamu vizuri hawa, wote ni moto wa kuotea mbali na kila mmoja yuko juu, hivi ushawahi kuona mafahari wawili wakakaa zizi moja? Nawaambia ipo siku mtasikia kimenuka, sisi tupo,” alisema mmoja wa wasanii aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jasmine Charles alisema kuwa, yeye alishawahi kuwa na urafiki na wasichana hao kwa nyakati tofauti lakini hawakudumu kutokana na tabia zao.

“Mimi nakwambia wote washawahi kuwa mashoga zangu lakini hatukudumu, sasa leo wameungana, huoni kuna harufu ya damu hapo?” Alihoji mrembo huyo na kuongeza;
“Siwaombei mabaya ila wanatakiwa kuwa makini tu katika kuiendesha kampuni yao kwa nidhamu na kuheshimiana, wamethubutu kufanya jambo la msingi, naamini watafanikiwa.”

Wakizungumzia madai hayo, masistaduu hao ambao tayari wameshaandaa filamu moja walisema kuwa, wanajua mengi yatasemwa lakini wao wako imara na watatimiza kile walicholenga.

Najua wataongea mengi ila hapa ni kazi tu, sisi wote ni mastaa, tumeamua kuungana ili tutimize ndoto zetu,” alisema Jack.

Naye Wema a.k.a Mrs Diamond alisema: “Wengi hawakutegemea kama sisi tunaweza kufanya kazi pamoja, sasa imekuwa na tunaamini hakuna cha harufu ya damu wala nini, tumedhamiria kuleta mabadiliko.”